A PHP Error was encountered

Severity: Notice

Message: Only variable references should be returned by reference

Filename: core/Common.php

Line Number: 272

MAKOSA YA RAMADHAN - SEHEMU YA 1 | Blog
Fun!

Insights

Kuna watu wanaohifadhi saum  zao za ramadhan, wanakithirisha ibada ikiwemo swala za faradhi kila mwaka na ‘Ibaadah nyingine. Lakini ‘Ibaadah zao huzipeleka ndivyo sivyo kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Nazungumzia watu wanaokwenda kwa waganga kupiga ramli, kuangalia bahati kwa kupitia ‘nyota’, na du’aa zao hawazielekezi kwa Allah moja kwa moja bali wanaomba mizimu, makaburi na kuvaa mahirizi wakitumai zitawakinga na madhara na shaitani, ihali Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amelikemea sana jambo hilo kwa kusema :

“Kama ukimshirikisha (Allah) bila shaka ‘amali zako zitaruka patupu, (hutozipatia thawabu japo ni ‘amali njema); na lazima utakuwa miongoni mwa wenye khasara.” Az-Zumar: 65

Na Amesema Allah Mtukufu:

“Hakika Allah Hasamehe kushirikishwa; na Husamehe yasiyokuwa hayo (ushirikina) kwa Amtakae. Na Anayemshirikisha Allah bila shaka amebuni dhambi kubwa.” An-Nisaa: 48 

Amesema tena Allah Mtukufu:

“Kwani anayemshirikisha Allah, hakika Allah Atamharamishia Pepo, na mahali pake ni Motoni. Na madhaalim hawatokuwa na wasaidizi (wa kuwasaidia siku ya Qiyaamah).” Al-Maaidah: 72

Hivyo basi mshirikina hatokubaliwa matendo yake  mpaka aache ushirikina atubie kwa Mola wake na ampwekeshe katika ‘Ibaadah zake ndio zitapokelewa amali zake.

* Na miongoni mwa watu wameufanya mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa kucheza na mambo ya upuzi, mwezi wa kupoteza wakati na kuifanya saum ni jambo jepesi bila mazingatio yoyote. Utawaona watu mchana wa Ramadhan na usiku wake wanacheza Karata, Keram, Dhumna, Bao na mfano wake. Wamejikusanya makundi kwa makundi wake kwa waume watoto kwa wazee wamechanganyika wala hawaoni hayaa, na wengine wameufanya ni mwezi wa kupiga ngoma, hasa ukiangalia katika nchi zetu za Afrika Mashariki; wanadai kupiga ngoma kuamsha watu kula daku, na wengine hucheza ngoma hizo hasa ikaribiapo siku ya Eid huanza kupiga ngoma zao mchana wa Ramadhaan wakiomba ‘Idi toa’, yaani wapewe pesa na huku wanaume wakiwa wamejivisha mavazi ya kike na kukata viuno hadharani!! Hawajui kuwa hiyo ni laana!

Kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) amesema:

“Allaah Amemlaani mwanaume anayejifananisha na mwanamke na mwanamke anayejifananisha na mwanaume”

Jamani huku ni kuudhalilisha Uislamu kwani dini hii si ya mchezo na magoma au kusikiliza miziki; hiyo sio ‘Ibaadah bali ni katika makosa makubwa kwa wanaocheza na wanaosikiliza na wanaoshangilia na kuwapa pesa hao waimbaji na wachezaji, kwani wote hao wanapata madhambi.

Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Amesema:

“Na katika watu wako wanaokhitari {kuchagua} maneno ya upuuzi (nyimbo na miziki) ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyeezi Mungu, pasipo wao kujua lolote, na wanaicheza shere hiyo njia ya Mwenyeezi Mungu. Basi hao watapata adhabu ifedheheshayo,
“Na wanaposomewa Aayah Zetu, huzipa mgongo kwa kujivuna kama kwamba hawakuzisikia, basi wape khabari ya adhabu iumizayo.” Luqmaan: 6-7

Hivyo ndugu zanguni hiyo sio dini ya kucheza wala kupiga ngoma za ‘daku kula” wala ‘Idi toa’ wao wanajiona wako katika dini, lakini hakika yote hayo wayafanyayo ni makosa. Wamesahau kuwa mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa ‘Ibaadah na Jihaad na kujivunia thawabu kwa wingi na kuacha mambo ya kipuuzi.

* Na miongoni mwa watu wameufanya mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa kulala na uvivu, wakesha kwa kula marungi na kuangalia vipindi vya kipuuzi kwenye TV. Vipindi vya vichekesho (Vunja Mbavu), Michezo ya Kuigiza (Tamthilia), Miziki (hususan wanayoiita ya vizazi vipya!), Masinema ya ovyo, na misalsalati. Kukesha usiku na kulala karibu ya alfajiri, wanalala mchana kutwa na kupitwa na swala ya Adhuhuri na Alasiri wanaamka karibu ya Magharibi kwa ajili ya kufuturu, kufanya kwao hivyo wajue kuwa wanachuma madhambi na hawapati kitu kwa Allaah, kwani wanafuata hawaa za nafsi zao na kuacha maamrisho ya Allaah (Subhanahu wa Ta’ala).

Wamesahau kuwa huu ni mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa jihaad ya nafsi kushindana na matamanio yote ya kipuuzi ili mtu apate kufuzu na asipitwe na fadhila za mwezi huu mtukufu.

* Na miongoni mwa watu wameufanya mwezi huu ni mwezi wa kula na kunywa na kushindana katika vyakula na kujifakharisha na vyakula vya kila aina kwa wakati mmoja, wanakula na kunywa wanashiba kupita kiasi mpaka wanashindwa kufanya ‘Ibaadah khasa ‘Ibaadah ya Taarawiyh,

Wamesahau kuwa mwezi huu ni mwezi wa kutoa na kuwalisha masikini. Kadhalika ni mazingatio ya kujikumbusha ‘Ibaadah hii ya kufunga ili kutambua shida ya kukaa na njaa kwa mwenye nacho kuwakumbuka waso nacho na sio kufanya Israfu na kujifakharisha.

* Na miongoni mwa makosa yanayofanywa na wanawake ni kuanza kuingia jikoni toka asubuhi; wanapika na kuandaa vyakula vya kila aina, anataka siku moja hiyo apike mahanjumati yote; sambusa, kababu, katles, kachori, kunde, maharage, chapati, maandazi, vibibibi, huku akisikiliza nyimbo badala ya kusikiliza Mawaidha, mpaka inafika robo ya Ramadhaan anaanza kujiuliza ‘nipike nini’ maana kila kitu keshapika! Kwa wakati mfupi ‘Ibaadah zinampita za kusoma Qur-aan, madarasa ya kumpandisha Iymaan ya kumuelimisha juu ya ‘Ibaadah yake yanampita hana nafasi, yeye anaandaa na kupika tu, na ifikapo Magharibi anaanza kupakua tu kuandalia waume, hata anachelewa kufungua Swawmu na Swalah ya Magharibi inampita au anaiswali kwa kuchelewa. Amesahau kuwa Swalah ni Waajib inapofika wakati wake.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amesema:

“Hakika ya swala kwa waumini imewekewa wakati maalum”

Na pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;

“Hawatowacha kuwa katika kheri umati wangu pindi watakapofanya haraka ya kufturu (kufungua Swawm) na kuchelewa kula daku”

Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) amesema;

“Mwenyeezi Mungu aliyetukuka Anasema: “Nampenda Mja wangu anapofanya haraka ya kufungua saum”

Na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) “Walimuuliza wanaume wawili katika Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) mmoja wao anachelewa kufuturu, na anachelewa kuswali, na mwengine anawahi kufuturu na anawahi kuswali, ni nani aliye bora? Akasema: ambaye anawahi kufuturu na anawahi kuswali ndio bora.” Muslim

Inapendeza kwa mwenye kufunga saum aharakishe kufungua pindi tu jua linapozama.

ITAENDELEA...

(Photo credits http://dontpaniciamislaamic.blogspot.com/)

Comments

There are no comments

Posting comments after has been disabled.