A PHP Error was encountered

Severity: Notice

Message: Only variable references should be returned by reference

Filename: core/Common.php

Line Number: 272

MAKOSA TUFANYAYO RAMADHAN - SEHEMU YA 2 | Blog
Fun!

Insights

* Na miongoni mwa watu wanaofunga saum zao vizuri lakini wanafungua saum ama wanafuturu kwa vitu vya haramu. Kwa mfano uvutaji sigara, tumbaku na uraibu mwengine ambao ni haramu si Ramadhan tu bali hata miezi mingine iliyosalia. Watu hao hustahi wakati wa mchana wa Ramadhan kwaajili wamefunga lakini wanaisubiri Magharibi kwa hamu na pakti ya sigara mkononi au mkebe wa tumbaku. Kitu cha mwanzo baada ya kuzama jua ni kufungua kinywa kwa haramu hizo. Hakika watu hao wamesahau au hawaijui hadith ya Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) iliyopokelewa na Anas (Radhiya Allaahu ‘Anhu):

“Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) alikua akifungua kwa Ratab, akikosa anafungua kwa Tende, akikosa anafungua kwa funda la maji.”

Inapendeza na ni Sunnah kufungua kwa tende au kwa maji na sio kufungua kwa vitu vilivyoharamishwa au hata vilivyo halali lakini si katika sunnah; huko ni kujikosesha thawabu na fadhila, pia harufu ya sigara mtu anapoingia msikitini huwakera watu na malaika.

* Na miongoni mwa watu kuna wale wanaoswali Taaraweh lakini wanachagua ni mahali gani pa kuswalia. Kwa mfano mahala ambapo huswalishwa haraka haraka kwa surah fupi fupi na kumalizika mara moja. Kadhalika wanaswali kwa uvivu na kukatakata swala zao, mara wanaswali mara wamechoka hawamalizi sambamba na Imamu. Utamuona mtu anaswali rakaa za mwanzo na anakaa kusubiri za mwisho. Huo ni uvivu wa ‘Ibaadah. Kuna na wengine hawaswali kabisa.

Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) amesema:

“Mwenye kusimama (kwa swala) mwezi wa Ramadhaan kwa imani na kutarajia malipo atasamehewa madhambi yake yaliyopita” Al-Bukhaariy na Muslim.

* Na miongoni mwa watu kuna wanaofunga saum kwa sababu ya mazowea au wanafunga kwa sababu nyumbani watu wote wanafunga au katika mji watu wanafunga anaona aibu kula mchana inabidi naye afunge, hafungi kwa niyah ya ‘Ibaadah na kuwa hiyo ni amri ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala), hali Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) amesema;

“Mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na akataraji malipo Mwenyezi Mungu humsamehe madhambi yake yaliyopita” Al-Bukhaariy na Muslim

* Na miongoni mwa watu kuna wanaofunga Ramadhaan lakini hawaachi yaliyokatazwa miongoni mwa mambo ya haramu kama kusengenya, kusema uongo, kutukana, kufitinisha watu na ushuhuda wa uongo kufanya ghushi (udanganyifu) ilhali mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Alihii wa Sallam) amesema:

“Yeyote ambae hatoacha kusema uongo, kusengenya, kufitinisha, kutoa ushuhuda wa uongo, basi ajue kuwa Allaah hana haja na Swawm yake katika kuacha chakula chake na kinywaji chake” Al-Bukhaariy Na Muslim

Hivyo basi inampasa kila Muislam awe makini na aachane na mambo kama haya na mfano wake hasa akiwa ndani ya Swawm, kwani hupelekea Swawm kuharibika na kukosa Thawabu na Fadhila za mwezi huu Mtukufu.

* Na miongoni mwa watu kuna wanaofunga mwezi wa Ramadhaan lakini hawaswali kabisa si swalah ya Taaraweh tu bali hata swalah za faradhi. Wengine huswali kwa kuchagua nyakati za swala na wengine wanaswali magharibi tu tena wanakwenda kwa kufuata mahanjumati misikitini na haya ni makosa ndugu zanguni, kwani kwa kufanya hivyo mtu ataingia katika kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) inayosema;

“Ole wao (adhabu kali) kwa wenye kuswali, ambao huzisahau (huzipuuza) swala zao, ambao hujionyesha (ili watu wawaone kua wao wanaswali).” Al-Ma’uun: 5-7

*Na miongoni mwa watu wengine huswali Ramadhaan hadi Ramadhaan au Ijumaa mpaka Ijumaa, inapomalizika Ramadhaan wanaacha kuswali.

Na mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) amesema:

“Swala tano, na Ijumaa hadi Ijumaa, na Ramadhaan hadi Ramadhaan, unasamehewa madhambi baina yake pindi utakapojiepusha na madhambi makubwa”

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) amesema:

“Kama mkijiepusha na madhambi (maovu) makubwa mnayokatazwa, tutakufutieni makosa yenu madogo na tutakuingizeni mahali patukufu (kabisa nako ni peponi).” An-Nisaa: 31

*Na miongoni mwa madhambi makubwa ni kuacha swalah kwa makusudi bila ya udhuru wa kishari’ah.. Maulamaa wamesema yule asiyeswali swalah tano hana saum kwa sababu mwenye kuacha swala ni Kaafir kwa kauli ya mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam):

“Baina ya mtu na kufru na shirki ni kuacha swala” Muslim

Na kaafir na mushrik hakubaliwi ‘amali zake’ kwa kauli ya Allaah Mtukufu:

“Na kama wangemshirikisha bila shaka yangaliwaharibikia yale waliyokuwa wakiyatenda” Al-‘An’aam: 88

* Na miongoni mwa watu wanafunga mwezi wa Ramadhaan kwa shime inapokuwa mwanzo wa mwezi, na wanafanya uvivu katika kumi la mwisho wakati kumi la mwisho ni bora kuliko la mwanzo, hasa utawaona kina mama hawana nafasi ya kufanya ‘Ibaadah kutwa wanahangaika madukani kuwatafutia watoto nguo za ‘Eid, wakirudi majumbani wamechoka hawawezi tena kusoma Qur-aan wala harakati nyingine za ‘Ibaadah. Wameufanya ni mwezi wa kuhangaika.

Wamesahau kuwa katika kumi la mwisho kuna usiku wa Laylatul Qadr usiku ulio bora kuliko miezi Elfu,
Amesema Allaah Aliyetukuka:

“Huo usiku wa hishima (huo) ni bora kuliko miezi elfu,
Huteremka malaika na Ruuh katika (usiku) huo kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo,
Ni amani (usiku) huo mpaka mapambazuko ya Alfajiri.” Al-Qadr: 2-5

Na mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) katika hadith iliyopokewa na mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha);

“Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam) linapoingia kumi la mwisho anakesha usiku, na kuwaamsha watu wa nyumbani kwake (wake zake), na anakaza shuka lake (yaani kukaza shuka makusudio kujitahidi kufanya ‘Ibaadah kwa wingi)” Al-Bukhaariy na Muslim

Amesema tena mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha):

“Hakuwahi kumuona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiisoma Qur-aan yote usiku mmoja, wala kusimama mpaka asubuhi, wala kufunga mwezi mzima katu isipokuwa Ramadhaan tu.” An-Nasaaiy

Mtume wa Allaah anajitahidi na kusoma Qur-aan yote kwa na hali ya kuwa yeye amesamehewa madhambi yake yaliyopita na yatakayokuja Je, mimi na wewe hizo juhudi tunazo na hali hatuna uhakika wa kusamehewa madhambi yetu?

* Na miongoni mwa watu kuna ambao hawaisomi Qur-aan, wala hawaswali, ispokuwa mwezi wa Ramadhaan tu. Akimaliza Ramadhaan kusoma na kuswali kumekwisha mpaka Ramadhaan nyingine ifike, kama vile kapewa ahadi na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuwa atafika Ramadhaan nyingine. Na miongni mwao wako ambao hawaijui Qur-aan kabisa si katika Ramadhaan wala miezi mingine, hao Mwenyeezi Mungu Amewaziba nyoyo zao na macho yao kwa matamanio ya nafsi zao kupenda Dunia kuliko Akhera yao.

“Na amesema ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu):
“Zingetwaharika nyoyo zenu endapo mngezishibisha maneno ya Allaah.”

Mwisho nawausia pamoja na kuiusia nafsi yangu kumcha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) na kujipinda kufanya ‘Ibaadah kama itakikanavyo na sio kufanya ‘Ibaadah mwezi u tu ukimalizika tunaacha. Tujitahidi tudumu katika kumtii Mola wetu Mtukufu, kwani Swawm inakulea na kukufanya udumu katika ‘Ibaadah pindi ukiifanya kwa ikhlaasw na sio kudharau kwani huu mwezi ni wa Jihaad ya kupambana na nafsi kutokana na vitimbi vya Shaytwaan, na ili tuweze kumshinda, tunapaswa kujikurubisha kwa Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) katika kumtii kwa Aliyotuamrisha na kujiepusha na Aliyotukataza.

Na tuseme kwa pamoja,

“Tumesikia Na Tunatwii” InshaAllaah

WabiLlaahit Tawfiyq
“Bila shaka Mwenyeezi Mungu hawapendi wenye kiburi na kujifakharisha” An-Nisaa: 36

(Photo credits http://dontpaniciamislaamic.blogspot.com/)

Comments

There are no comments

Post a comment