Current Affairs
Serikali ya Kenya imetoa agizo la kutotoka nje usiku (kuanzia 6.30pm hadi 6.30am) kwa wakaazi wote wa kaunti ya Lamu iliyoanza kutekelezwa tarehe 20/07/2014 (kwa kipindi cha mwezi mmoja), kama mojapo ya mbinu za kupambana na ongezeko la ukosefu wa usalama katika eneo hilo la Pwani ya Kenya.
Agizo hilo ambalo litatekelezwa kwa muda wa mwezi mmoja linaelekea kutopokelewa vyema na ndugu waislamu ambao ni asilimia kubwa ya wakaazi wa kaunti ya Lamu. Hilo hasa linachangiwa na uhalisia wa kwamba agizo hili limetolewa katika ‘kumi la mwisho’ la mwezi mtukufu wa Ramadhan; kipindi ambacho ndugu waislamu huzidisha ibada na hata kukesha misikitini kwa ajili ya swala.
Wakati wa mwezi mtukufu wa ramadhan, waumini huhitajika kuzidisha ibada kwa minajil ya kupokea toba na vilevile kujikurubisha karibu zaidi na mwenyezi Mungu.
Basi hapo ndipo agizo la serikali ya Kenya linapoelekea kuonekana kuingilia uhuru wa ibada, hususan ikizingatiwa kwamba wakaazi wengi wa kaunti ya Lamu ni waislamu ambao wanafunga mwezi huu wa Ramadhan. Kuwanyima haki ya kwenda kwa swala muhimu zikiwemo zile za Tarawweh na Tahajjud huenda kukaiweka serikali pabaya kwani ibada ni haki ya kikatiba ya kila mkenya.
Siku ya Jumatatu tarehe 21/07/2014, Kimaiyo alikua na kikao na kamati ya usalama kutoka bunge la kaunti ya Lamu, viongozi wa kisiasa na wa kiislamu kujadili suala hilo. Iliafikiwa kuwa waislamu hawatoathiriwa na marufuku hiyo na wataruhusiwa kuendelea na ibada za mwezi wa Ramadhani. Hatahivyo, kuna fununu kuwa wenyeji wa Mkunumbi walihangaishwa usiku wa 21/07/2014.
Idara ya polisi imetuhumiwa mara kadhaa kwa kukiuka haki za kibinaadamu na kikatiba. Siku chache zilizopita (tarehe 14/07/2014) Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Huduma za Polisi (IPOA) ilizindua ripoti yake kuhusu zoezi la kukabiliana na ugaidi mtaani Eastleigh jijini Nairobi maarufu "Usalama Watch." Ripoti hiyo ilibainisha kuwa oparesheni nzima ilikabiliwa na visa vya dhuluma. Hadi hii leo kuna watu waliofungwa katika mazingira duni katika seli ya Kasarani.
Ukweli ni kwamba usalama ni muhimu kwa kila mkenya, na ni jukumu la seriklai kuhakikisha usalama huo unapatikana kwa kila mtu. Hata hivyo, juhudi za kudumisha usalama hazipaswi kamwe kuzuia uhuru wa kikatiba wa ibada. Aghalabu itafaa zaidi kwa serikali kuhakikisha inadumisha usalama lakini pia kuwaruhusu ndugu waislamu wa kaunti ya Lamu waendelee na ibada yao msimu huu wa ramadhan.
There are no comments