A PHP Error was encountered

Severity: Notice

Message: Only variable references should be returned by reference

Filename: core/Common.php

Line Number: 272

AHMAD NASSIR | Blog
Fun!

Insights

 AHMAD NASSIR JUMA BHALO alizaliwa tarehe 27/5/1936 mtaani Kuze mjini Mombasa. Mzee huyu anatoka katika kabila la Waswahili,  kwa upande wa babake ni Mtangana na kwa upande wa mamake ni Mkilindini. Hizi ni miongoni mwa kabila za asili ya Kiswahili za ki-mvita, yaani Mombasa.

Kama watoto wengine wa Kimombasa wa wakati huo alibahatika kupelekwa chuoni (Madrassa) aliposoma Kuraani

Ustadh Ahmad Nasser


(Qur'an) pamoja na masomo mengine ya dini ya Kiislamu. Mafunzo hayo aliyapata kutoka kwa babu yake Sheikh Muhammad Ahmad Matano, mpaka kuhitimu kwake.

 Baada ya mafunzo hayo, alijiunga na shule ya msingi ya Arab Boys ( Siku hizi inajulikana kama shule ya msingi ya Serani) mjini Mombasa kwa masomo ya dunia. Hatahivyo hakumaliza masomo yake na aliwata (aliwacha) akiwa darasa la nne, na akaanza kufanya kazi. 

 Bwana huyu ni mshairi mashuhuri katika uwanda (uwanja) wa mashairi, anajulikana sana kwa jina la Ustadh Bhalo. Bhalo ni lakabu ya babu yake mzaa baba yaani Juma Bhalo, na Ustadh ni cheo alichopewa na mhariri wa gazeti moja la Mombasa lililokuwa likiitwa SAUTI YA PWANI, baada ya kupata diploma yake ya ushairi. 

 UTUNZI WA MASHAIRI 

 Lugha anayotumia Ahmad Nassir kutungia mashairi yake ni ile ya kiswahili tena cha ndani. Kwa sababu hii, si rahisi kwa mtu mwenye ujuzi mdogo wa lugha ya Kiswahili kuyaelewa mashairi yake bila ya usaidizi. Mtu yeyote anaesoma mashairi yake akaona jinsi anavyotezea (anavyochezea) lugha ataelewa kuwa bwana huyu amekwasika kilugha na ni bingwa kweli. 

Mpaka sasa ametunga mashairi mengi sana, na bado anaendelea kutunga licha ya umri wake mkubwa. Baadhi ya mashairi hayo yamechapishwa na mengine bado yanasubiri kuchapishwa. Mashairi yake yake mengine yameimbwa na Mohamed Khamis Juma Bhalo Al maaruf Professor Juma Bhalo (Mungu amrahamu) katika nyimbo zake za taarabu, wawili hawa ni mtu na bin ammi yake. 

 Mashairi yake ya kwanza kuchapishwa ni yale yaliyomo katika kitabu kiitwacho` POEMS FROM KENYA’ kilichochapishwa na idara ya uchapishaji ya chuo kikuu cha Wisconsin nchini Amerika mnamo mwaka wa 1966. Mashairi hayo yalifasiriwa kwa kiingereza na kuhaririwa na mwenda zake Profesa Lyndon Harries wa Chuo Kikuu cha Wisconsin.

 Kitabu cha pili cha mashairi yake ni kile kiitwacho MALENGA WA MVITA, hiki kimehaririwa na Shihabuddin Chiraghdin (Mungu amrahamu) na kupigwa chapa na idara ya uchapishaji ya Chuo Kikuu cha Oxford University, humu nchini Kenya. Kitabu hicho kilipelekea kwa bwana Ahmad Nassir kutunukiwa  tuzo ya Kenyatta ya Fasihi ya Kiswahili mwaka 1972 kwa kuwa ni kitabu bora zaidi kuwahi kutolewa mwaka huo.

 Tuzo nyingine aliyoipata kwa umalenga wake ni "The Guiness Stout Effort award.' Tuzo hii ilimpatia shahada maalum pamoja na kikombe cha ushindi kilichoundwa kwa fedha. Vitabu vyake vengine vilivyofwata baada ya Malenga wa Mvita ni Taa ya Umalenga pamoja na Irshad. 

 Hivi sasa Bwana Ahmad yumo katika harakati za kuchapisha vitabu vengine viwili vikiwemo Kandi ya Lugha pamoja na Utenzi wa Fumo Liyongo vitakavyohaririwa na Abdilatif Abdalla nchini Ujerumani.

 Kuhusu mashairi yake ambayo hayajachapishwa ni mengi sana. Mbali na mashairi aliyonayo mwenyewe, kuna mengine kadha wa kadha yaliyo kwenye maktaba za vyuo vikuu mbali mbali ulimwenguni kama Ujerumani, Dar es salaam, London na hata Urusi ambapo yanatumiwa kwa masomo ya Ushairi.

 Mbali na uweledi wa mashairi bwana Ahmad Nassir ana kipawa cha uchoraji. Miongoni mwa kazi zake za uchoraji ni zile zilizokuwa katika vifua vya baadhi ya fulana za nyakati hizo za nyuma, kama zile za; Cruel world,Cruel hand, please kiss me na make love not war 

Comments

There are no comments

Post a comment